Utenzi wa Bikira Maria unapoimbwa na maskini, utamu wake unaongezeka!

Written by on August 18, 2017

Utenzi wa Bikira Maria yaani “Magnificat” una sheheni maneno yanayochochea uhuru wa kweli na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Ni utenzi unaofutilia mbali mifumo ya ubaguzi na unyanyasaji; ukosefu wa haki msingi za binadamu; kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema; upendo na mshikamano wa dhati! Ni utenzi unaokazia utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Unakazia upendo na mshikamano wa kidugu kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Mungu wanaopaswa kuishi katika misingi ya haki, amani na maridhiano.
Haya yamesemwa hivi karibuni na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, wakati alipokuwa anachangia mada kwenye kongamano la Kimataifa la Ibada kwa Bikira Maria, huko Aparecida, Kanisa nchini Brazil linapoadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 300 tangu Sanamu ya Bikira Maria wa Aparecida ilipookotwa na wavuvi, huo ukawa ni mwanzo wa Ibada kubwa kwa Bikira Maria kwa watu wa Mungu Amerika ya Kusini. Kardinali Amato anafafanua kwamba, dimbwi kubwa la umaskini wa hali na kipato ni changamoto kwa watu wa Mataifa kujenga uwezo wa kusaidiana kwa kujikita katika ukarimu unaoratibiwa na kanuni auni; kwa kujenga mshikamano na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

 
Huu ni wakati wa kuanzisha mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya maskini; mwelekeo sahihi wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ziwe ni mahali pa ushuhuda wa upendo na ukarimu. Waamini watambue kwamba, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa. Uhusiano kati ya umaskini na Kanisa unafumbatwa kwa namna ya pekee na imani kwa Kristo Yesu. Umaskini ni chachu muhimu sana katika mchakato wa kulipyaisha Kanisa kwa kuzingatia mambo msingi yanayotoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi; kwa utu na heshima ya binadamu. Umaskini ni kielelezo kinachochota umuhimu wake katika Fumbo la Umwilisho.

 
Utenzi wa Bikira Maria ni wimbo wa umaskini wa maisha ya kiroho unaoelezea jinsi ambazo Mwenyezi Mungu anapenda kutekeleza historia ya ukombozi wa mwanadamu, kwa kuwainua wanyonge na kuwapandisha maskini. Kristo Yesu, Mwana wa Mungu alithubutu kuzaliwa katika Pango la kulishia wanyama huko Bethlehemu, akaishi mjini Nazareti, maeneo ambayo hayakuwa na umaarufu wowote. Yesu katika maisha na utume wake, alijifananisha na maskini, akawapatia kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake, dhamana inayoendelezwa na Mama Kanisa hata katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Huu ni umaskini unaomwezesha mwamini kujiaminisha kwa tunza na ulinzi wa Mungu. Bikira Maria ni kioo cha maisha na utume wa Kanisa, unofumbatwa katika Injili ya upendo kwa maskini.

 
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu aliwahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu kwa kumwilisha ndani mwao matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji. Hii ndiyo Injili ya upendo inayofumbatwa katika utamaduni wa mshikamano unaozima kiu ya mahitaji msingi ya binadamu.

 

Kanisa katika mazingira ya Amerika ya Kusini, halina budi kukuza na kudumisha utamaduni wa upendo na mshikamano wa dhati kama kikolezo cha uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni mfano wa maisha yaliyoshuhudiwa na watakatifu mbali mbali kutoka Amerika ya Kusini. Hawa wamekuwa ni chachu ya upyaisho wa Kanisa mintarafu mchakato mzima wa utamadunisho, kiasi kwamba, Bikira Maria anaonekana kuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa imani na matendo yake.

 
Utenzi wa Bikira Maria ni Katiba ya watu wa Mungu, chemchemi ya furaha na nguvu ya Mungu inayookoa. Kwa mwelekeo huu, Bikira Maria ni kielelezo cha sauti ya kinabii; mwanamke jasiri na mwenye nguvu anayependa kushirikiana kwa dhati kabisa na Mwenyezi Mungu katika mapambano ya ukombozi wa mwanadamu. Utenzi huu ni chachu ya mageuzi ya maisha ya kiroho na kiutu yanayofumbatwa katika huruma ambayo kimsingi ni haki ya Mungu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.


Current track
TITLE
ARTIST

CLOSE
CLOSE