Rais MAGUFULI; Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa katika kudumisha Amani na Upendo na kuwaletea Wananchi maendeleo.

Written by on November 7, 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. JOHN POMBE MAGUFULI amelipongeza Kanisa Katoliki kwa mchango lililoutoa kuwahudumia Watanzania Kiroho na Kimwili tangu miaka 150 iliyopita, na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa katika kudumisha Amani na Upendo na kuwaletea Wananchi maendeleo.

Rais MAGUFULI amesema hayo wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, ambayo yamefikia kilele chake jana mjini BAGAMOYO Jimbo katoliki MOROGORO eneo ambalo Ukristo ulianzia.

Amewashukuru Maaskofu, Mapadre, Watawa na viongozi wote wa Kanisa Katoliki, kwa namna wanavyoshirikiana na Serikali na Madhehebu mengine ya dini katika kuleta maendeleo na kuimarisha ustawi wa jamii bila kubagua na amewaomba waendelee kukemea vitendo viovu vikiwemo uvunjifu wa amani, rushwa, ufisadi na ubakaji.

Aidha, Rais MAGUFULI amewashukuru Wananchi wa BAGAMOYO kwa kuupokea UKRISTO, ambao uwepo wake umeleta manufaa makubwa kwa Watanzania na ameahidi kuwa Serikali itashirikiana na Viongozi wa Kanisa hilo kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Naye Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Mhashamu GERVAS NYAISONGA amemshukuru Rais MAGUFULI kwa kuungana na Kanisa Katoliki katika Jubilei hiyo, amempongeza kwa kazi nzuri ya kutimiza ahadi alizozitoa kwa Watanzania katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake, na ameahidi kuwa Kanisa Katoliki litaendelea kuliombea Taifa na kushirikiana na Serikali.

 

Misa Takatifu ya Maadhimisho ya Jubilei hiyo ambayo imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa dini, Serikali, vyama vya siasa, na Watawa, na Waamini wale kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini, imeongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la NAIROBI NCHINI KENYA Kardinali JOHN NJUE, ambaye amemwakilisha Baba Mtakatifu FRANCISKO katika maadhimisho haya.

 


Current track

Title

Artist

CLOSE
CLOSE