Papa akumbusha kuhusu utu, heshima na haki msingi za binadamu!

Written by on January 9, 2018

Takwimu zilizotolewa na Sekretarieti kuu ya Vatican zinaonesha kwamba, hadi kufikia tarehe Mosi Januari 2018, Vatican ilikuwa na uhusiano wa kidiplomasia na nchi 185 na kati yake kuna Umoja wa Ulaya na Shirika la Kijeshi la Malta ambalo linadhamana na wajibu wa kulinda imani sanjari na kutoa huduma kwa maskini, wagonjwa na wahitaji zaidi. Mwaka 2017, Myanmar ilianzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican.
Kuanzia tarehe Mosi Januari 2017 hadi tarehe 7 Januari 2018, Baba Mtakatifu Francisko amepokea hati za utambulisho kutoka kwa mabalozi 31 na kati yao kuna Mabalozi wakazi 17. Nchi zenye Mabalozi wakazi kutoka Afrika waliowasilisha hati zao za utambulisho ni kutoka: Ghana, Misri, Nigeria na Afrika ya Kusini. Kwa ujumla, kuna mabalozi wanawake 25 wanaowakilisha nchi zao mjini Vatican kati yao 12 ni Mabalozi wakazi. Mabalozi 13 si wakazi, kwani wanatekeleza dhamana na wajibu wao wakiwa nje ya Roma. Kutoka Barani Afrika ni Mabalozi wa: Burundi, Gambia, Guinea, Guinea Bissau, Mauritania na Zimbabwe. Itakumbukwa kwamba, Vatican ina uhusiano wa kidiplomasia na Mashirika ya Kimataifa kama vile Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, kwa kutambua kwamba, huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji ni kati ya shuhuda zinazopaswa kutolewa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za wakimbizi na wahamiaji. Vatican pia ina uhusiano wa kidiplomasia na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM.
Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao kama mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, kama sehemu ya mapokeo ya kutakiana heri na baraka kwa Mwaka Mpya 2018, Jumatatu, tarehe 8 Januari 2018, amekazia umuhimu wa mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa katika kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kuibuka kila kukicha! Vatican kwa upande wake inapania kukuza na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi: kiroho na kimwili. Jumuiya ya Kimataifa kwa mwaka 2018 inaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 100 tangu kusitishwa kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia iliyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao na kwamba, kuna haja ya kujenga na kudumisha amani duniani inayofumbatwa katika ukweli, haki, mshikamano tendaji na uhuru mambo msingi yanayobainishwa kwenye Tamko la Haki Msingi za Binadamu, ambalo, kwa Mwaka huu, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu kuchapishwa kwake!
Baba Mtakatifu amekazaia umuhimu wa mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu kama msingi wa kukuza na kudumisha amani duniani. Dhamana hii inaweza kutekelezwa kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Amegusia changamoto ya amani huko Mashariki ya Kati na katika baadhi ya nchi za Kiafrika. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amefafanua tunu msingi za maisha ya kifamilia, changamoto zinazozikabili familia, yaani umaskini, vita na wimbi kubwa la wahamiaji pamoja na kazi za suluba wanazofanyishwa watoto wadogo. Baba Mtakatifu anabainisha mambo msingi yanayoweza kutumiwa na Jumuiya ya Kimataifa katika kupambana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani yaani kwa: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha. Amezishukuru nchi mbali mbali zinazojitahidi kutoa hifadhi na huduma endelevu kwa wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, kuna haja ya kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.
Professa Agostino Giovagnoli kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Milano anasema, hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko kwa mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kwa Mwaka 2018 imejikita hasa katika misingi ya: haki na amani; utu, heshima na haki msingi za binadamu; huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji pamoja na changamoto kubwa ya kuthibiti utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha duniani. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi kama sehemu ya utambulisho wa Bara la Ulaya na ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaotolewa na Mama Kanisa. Ukarimu kwa wageni utawawezesha wananchi wa Bara la Ulaya kutambua na kuthamini utambulisho wao! Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu Tamko la Haki Msingi za Binadamu lilipotolewa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Jambo la msingi ni kuwa macho dhidi ya “Haki Mpya” zinazoibuliwa na baadhi ya nchi kiasi cha kupingana na mila, desturi, utu na heshima ya binadamu.
Ni haki ambazo zinachochea utamaduni wa kifo na kumong’onyoa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kanuni maadili na utu wema! Haki msingi za binadamu zitumike kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii kimataifa na wala si chanzo cha kurejesha tena ukoloni katika baadhi ya nchi maskini duniani! Baba Mtakatifu amekazia haki, amani na maridhiano kati ya watu yanayotekelezwa katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Amani ya kudumu inafumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Hii ni amani shiriki inayowambata na kuwafumbata wote; amani inayoheshimu mazingira, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ut una heshima ya binadamu. Hotuba za Baba Mtakatifu Francisko zinatoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.


Current track
Title
Artist

CLOSE
CLOSE