Mapadre endelezeni maisha na utume wenu katika shule ya Bikira Maria

Written by on August 18, 2017

Dhamana na utume wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wareno unafumbatwa katika utambuzi kwamba, hii ni jumuiya ya Mapadre walio hai, wanaojisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa mahalia pamoja na Kanisa la kiulimwengu. Ni mahali pa majiundo ya awali na endelevu katika maisha na utume wa Wakleri, kwa kujichimbia kwenye shule ya Bikira Maria. Kwa njia hii, Mapadre wanaweza kuishi kama mitume na mahujaji wa imani wanaomfuasa Kristo Mchungaji mwema. Mapadre wawe ni vyombo na mashuhuda wa ukarimu, imani na matumaini kama yalivyoshuhudiwa na Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni huko Fatima, Ureno na Askofu mkuu Jorge Carlos Patròn Wong, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri anayeshughulikia majiundo ya Majandokasisi, alipokutana na kuzungumza na waseminari pamoja na mapadre ambao wamesoma katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wareno. Amekazia pamoja na mambo mengine, tasaufi ya Ibada kwa Bikira Maria hasa katika eneo hili ambalo kuna umati mkubwa wa familia ya Mungu katoka sehemu mbali mbali za dunia unafika kwa ajili ya kufanya hija ya maisha ya kiroho, kupitia kwa Bikira Maria, ili waweze kumwendea Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia.
Bikira Maria amekuwa ni hujaji wa kwanza katika historia nzima ya ukombozi wa mwanadamu, pale alipokubali kwa moyo radhi kabisa kushiriki katika mpango wa Mungu kwa ajili ya ukombozi wa binadamu, kiasi cha kujiaminisha mbele ya Mungu na kupokea kwa wasi wasi na furaha kubwa ujumbe kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu. Akajulishwa kwamba, binamu yake Elizabeti, amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake, yeye aliyeitwa tasa! Kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana mbele ya Mwenyezi Mungu. Bikira Maria akaondoka kwa haraka kwenda kumhudumia binamu yake, kielelezo makini cha mtume wa Bwana aliyejisadaka bila ya kujibakiza, kiasi hata cha kudiriki kusimama chini ya Msalaba na kupokea maiti ya mwanaye mpendwa, Kristo Yesu!
Bikira Maria ni mfano na kielelezo cha imani ambaye amediriki kuwa ni mfuasi wa Mwanaye mpendwa Yesu Kristo na jirani zake, huu ndio mtindo na mfumo wa maisha anaopaswa kuutekeleza na Padre. Daima mapadre wajitahidi kukua na kukomaa katika imani, matumaini na mapendo; sanjari na kuendelea kujikita katika majiundo endelevu ili kuboresha huduma yao kwa watu wa Mungu. Seminari na nyumba za malezi ziwe ni mahali ambapo si tu majandokasisi na mapadre wanapata mahali pa kufundwa kikamilifu, bali pawe ni mahali pa ushuhuda wa maisha na utume wa Kipadre; mahali ambapo wanajumuiya wanajenga na kuimarisha mahusiano yao ya kiutu na maisha ya kiroho: kwa kushirikishana:

 

maadhimisho ya mafumbo ya Kanisa, Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na huduma makini inayowatambulisha kuwa wao kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa waja wake. Kwa njia hii, mapadre wanaweza kujenga na kuimarisha umoja, udugu na upendo wao wa kikasisi. Hili ndilo lengo kuu ambalo linapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Padre anasema, Askofu mkuu Jorge Carlos Patròn Wong. Mapadre wawe na kiu ya upendo kwa Mungu na jirani zao, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza katika maisha na utume wa kipadre. Watambue kwamba, wao ni madaraja, mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake; mambo ambayo wanapaswa kuwashirikisha wale wote wanaokutana nao katika safari ya maisha na utume wao kama Makuhani.
Amekazia umuhimu wa utekelezaji wa Mwongozo mpya wa Malezi na majiundo ya Kipadre uliochapishwa tarehe 8 Desemba 2016, katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya asili. Malezi ni mchakato endelevu unaopania kumfunda jandokasisi katika maisha ya kiutu, kiroho, kiakili na kichungaji. Mang’amuzi na uzoefu huu unamwilisha hatua kwa hatua katika maisha ya jandokasisi na hatimaye, kukwekwa wakfu kama Padre. Ni changamoto kwa Mapadre kuhakikisha kwamba, majiundo makini wanayoyapata wakiwa seminarini na nyumba za malezi yanamwilishwa kwa kufumbatwa na kipaji cha ugunduzi, kwa kusoma alama za nyakati ili kutambua mahitaji msingi ya familia ya Mungu wanayoihudumia.
Mapadre katika maisha na utume wao, wajitahidi kukuza na kudumisha udugu wa kisakramenti wakitambua kwamba, wao wanaunganishwa na kuwa wamoja kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, inayoimarishwa kwa Kipaimara pamoja na Daraja Takatifu ya Upadre. Udugu huu hauna budi kupaliliwa kwa maisha ya kiroho, kwani hata Mapadre wanapaswa kuwa na washauri wao wa maisha ya kiroho, jambo linalokaziwa sana kama sehemu ya majiundo endelevu ya Wakleri. Mapadre wapatemuda wa kujitenga na malimwengu kwa ajili ya sala, mafungo na tafakari; wasaidiane kwa hali na mali ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika maisha na utume wao kama Mapadre.
Hizi ni changamoto za kiimani, kitamaduni na katika shughuli za kichungaji. Mapadre waangalie wasitumbukie katika upweke hasi unaoweza kuwasababishia kukosa ari na mwamko wa maisha na utume wa Kipadre na matokeo yake na kuitema zawadi na wito wa Kipadre. Majiundo ya Kipadre ni dhamana endelevu inayofikia ukomo wake, pale Kasisi anapoitupa dunia mkono, ili kwenda kwenye pumziko la maisha ya milele. Mapadre wawe ni mwono wa huduma kwa ajili ya Makanisa mahalia lakini pia wakumbuke kwamba, wanatumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wote wa Mataifa. Nyumba za malezi zinazowaunganisha Mapadre kutoka sehemu mbali mbali za dunia, iwe ni fursa ya kushirikishana maisha na utume wa Kipadre.
Askofu mkuu Jorge Carlos Patròn Wong, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri anayeshughulikia majiundo ya Majandokasisi anahitimisha tafakari yake kuhusu majiundo endelevu kwa Mapadre kwa kusema kwamba, nyumba za malezi endelevu ni shamba la mitume linalowasaidia Mapadre kukua na kukomaa zaidi katika maisha na utume wao, ili hatimaye, wawe kweli ni wachungaji, mashuhuda na vyombo vya Injili; kwa kukuza na kudumisha udugu wa Kikuhani kwa ajili ya huduma kwa Kanisa mahalia na Kanisa la Kiulimwengu!


Current track
Title
Artist

CLOSE
CLOSE