Maadhimisho ya Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu nchini Ghana

Written by on August 8, 2017

Maadhimisho ya Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa huko katika Jimbo Katoliki la Jasikan, Ghana kuanzia tarehe 7 Agosti hadi tarehe 13 Agosti, 2017 ni sehemu ya  utekelezaji wa mikakati ya shughuli za kichungaji iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu umuhimu wa Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ni kipindi cha katekesi ya kina kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, Sala na tafakari ya kina inayofanywa na Jumuiya ya waamini wa Kanisa mahalia mintarafu Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kama njia ya kuendelea kuzungumza na Kristo katika safari ya maisha ya waamini. Ni muda wa kuimarisha katekesi kuhusu Sakramenti ya Upatanisho, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

 

Ekatisti Takatifu na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni tema zinaofanyiwa kazi wakati wa Makongamano ya Ekaristi Takatifu, sehemu mbali mbali za dunia. Ekaristi na huduma makini kwa maskini ni mada ambayo inaendelea kupewa uzito wa juu hasa baada ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya Huruma ya Mungu ambamo Baba Mtakatifu Francisko amenzisha Siku ya Maskini Duniani. Upendo ni sumaku inayomuunganisha Mungu na binadamu, changamoto ya kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Leo hii, maskini wanaonekana kuwa ni kero kwa Jumuiya ya Kimataifa, watu wasiokuwa na utu wanaochezewa kama “mpira wa danadana” na kukandamizwa chini kama “soli ya kiatu”! Ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mahangaiko ya maskini na akina “yakhe pangu pakavu tia mchuzi”, ameamua kuanzisha Siku ya Maskini Duniani, itakayoadhimishwa na Mama Kanisa kuanzia sasa kila Jumapili ya XXXIII ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa, kabla ya maadhimisho ya Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu inayofunga rasmi maadhimisho ya Mwaka wa Liturujia wa Kanisa.

 

Siku ya Maskini Duniani inapaswa kuwa ni siku ya kutafakari jinsi ya kumwilisha huruma na upendo wa Mungu kwa maskini, kwa kujenga na kudumisha matendo ya huruma: kiroho na  kimwili. Huu utakuwa ni mwendelezo sahihi wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kipindi cha neema na baraka. Ni wakati wa kufungua akili na nyoyo za watu ili kuangalia ni kwa jinsi gani huruma ya Mungu inaweza kumwilishwa katika matendo ya huruma kama kielelezo cha imani tendaji na ushuhuda wenye mvuto na mashiko wa uinjilishaji mpya.

 

Upendo unaongoza, sheria inatekeleza! Si haba kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana, limeamua kuweka mada hii kama sehemu ya tafakari ya kina wakati wa maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa. Ekaristi Takatifu na Familia ni mada inayowakumbusha waamini kwamba, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya upendo, ni chakula cha kweli kilichoshuka kutoka mbinguni! Ekaristi ni Yesu mwenyewe, Mwanakondoo kweli wa sadaka ya Agano Jipya na la milele. Ni kanuni sababishi ya uwepo wa Kanisa na kwamba, Ekaristi Takatifu inajenga Jumuiya ya Kikanisa. Ni Sakramenti ya Bwana na Bibi Arusi inayo imarisha umoja na upendo usiovunjika ndoa ya Kikristo. Hapa familia inakuwa kweli ni Kanisa dogo la nyumbani, eneo la kwanza kabisa la maisha ya Kanisa linaloweka msingi wa malezi na makuzi ya tunu msingi za maisha ya Kikristo, kiutu na kitamaduni. Familia ni madhabahu ya Injili ya uhai kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, kwani Ekaristi ni umoja na upendo wa daima!

 

Maadhimisho haya ni kipindi ambacho waamini wanakuza na kudumisha Ibada mbali mbali kwa Ekaristi Takatifu kadiri ya Mafundisho ya Kanisa, wakipania kumwilisha uwepo wa Kristo kati yao katika tafakari ya kina ya shughuli za kichungaji na ushuhuda wa maisha yao ndani ya jamii. Zaidi ya waamini elfu kumi wanatarajiwa kushiriki kikamilifu katika tukio hili muhimu linaloonesha pia umoja na mshikamano wa familia ya Mungu nchini Ghana. Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Ghana kwa mwaka 2017 linaongozwa na kauli mbiu “Ekaristi Takatifu na Uinjilishaji Mpya”.

 

Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha upendo wa hali ya juu kabisa unaofumbatwa katika huduma ya upendo kama alivyofanya Yesu Kristo mwenyewe siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, alipoiweka Sakramenti hii pamoja na kuwaosha miguu wanafunzi wake, kielelezo cha huduma makini, dhana iliyotiliwa mkazo na Baba Mtakatifu Francisko wakati na baada ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu. Huduma makini ni kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji, inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

 

Waamini wanakumbushwa kwamba, ni kwa njia ya maadhimisho ya kina ya Fumbo la Ekaristi Takatifu wanapata fursa ya kujenga na kuimarisha uhusiano kati yao na Kristo, hapo hapo wakijitahidi kujenga mahusiano mema na jirani zao. Kwa maneno mengine, hii ndiyo inayopaswa kuwa ni taswira ya Kanisa la Kristo katika ulimwengu mamboleo. Ekaristi takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; ni chanzo na uwepo endelevu wa Kanisa na matokeo yake yanajionesha kwa namna ya pekee katika maisha na utume wake.

 

Waamini licha ya kusali na kutafakari juu ya ukuu na utakatifu wa Fumbo la Ekaristi Takatifu, wanafanya maandamano makubwa wakiwa wamebeba Ekaristi, kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo miongoni mwa wafuasi wake; kwa hakika, hiki ni kipindi cha kujenga umoja na mshikamano wa Kikanisa, kwa kuhimiza wongofu wa ndani, toba na msamaha wa kweli. Ni mwaliko wa kuvuka vikwazo na migawanyiko ili kujenga tena Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Fumbo la Ekaristi Takatifu lina nguvu kubwa ya kuwaunganisha waamini katika imani na matumaini ya kweli.

 

Yesu wa Ekaristi anaendelea kuwalisha wafuasi wake katika umoja, daima akiwataka wajipatanishe na Mungu pamoja na jirani zao. Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana, linaadhimisha Kongamano la Ekaristi Takatifu kama alama ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kuadhimisha Jubilei ya miaka 60 ya uhuru wa Ghana na mahusiano ya kidiplomasia na Vatican, tayari kusima kidete kulinda, kutunza na kudumisha haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, huku utu na heshima ya binadamu vikipewa msukumo wa pekee kabisa. Matukio yote haya anasema Askofu Gabriel Mante wa Jimbo Katoliki Jasikani, Ghana, mwenyeji wa Kongamano hili kwamba yanapania kuwajengea waamini upendo kwa Fumbo la Ekaristi takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kanisa Katoliki nchini Ghana linaundwa na Majimbo 20 yanayowakilishwa walau na waamini kumi kutoka katika kila Jimbo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

 


Current track
Title
Artist

CLOSE
CLOSE