Leo Machi 9, Kanisa linamkumbuka Mtakatifu Fransiska wa Roma Mtawa na mwanzilisi wa Shirika

Written by on March 9, 2018

Leo Kanisa linamkumbuka Mtakatifu Fransiska wa Roma Mtawa na mwanzilisi wa Shirika

Fransiska alizaliwa Roma (Italia), mwaka 1384. Aliolewa akiwa na umri wa miaka Kumi na Mitatu, alizaa Watoto sita, wawili kati ya hawa wallikufa wakiwa bado wachanga. Siku za mwanzo Fransiska alikuwa akikaa raha mustarehe kwao katika mji wa Roma. Baadaye alipatwa na msiba. Kwanza vita vilipotokea mume wake alipelekwa ugenini, halafu mwanawe alitolewa kwa maadui kama amana. Alinyang’anywa mali zote na jumba lilibomolewa. Lakini Fransiska hakukata tamaa katika uchungu huo. Alikaa imara akazidi kumpenda Mungu. Aliporudishiwa mali zake, nyingine alizigawa kwa maskini na nyingine alizigawa zitumike kwa huduma nyingine njema.
Mwaka 1425 alianzisha Shirika la “Waoblati”,waliofuata Kanuni ya MT.Benedikto. Kisha kufa kwa mume wake, Fransiska aliingia mwenyewe katika Shirika lile. Kwa kuwa alikua mwanamke Mtakatifu sana, alijaliwa na Mungu kumwona Malaika mlinzi wake kutwa kucha karibu naye. Malaika huyo alig’aa uso kwa furaha. Alikuwa na nywele ndefu zenye rangi ya dhahabu, kanzu aliyovaa ilifumwa kwa maua meupe. Alimsindikiza kila mahali,akimtia shime katika masumbuko. Fransiska alipokosa,Malaika alimkaripia. Siku moja Fransiska alialikwa kwenye karamu, Watu waliokaa mezani karibu naye katika hiyo karamu walianza kuwasengenya na kuwachongea watu bure. Fransiska alikaa kimya asiwakaripie wachongezi wale, Basi Malaika wake alimpiga kofi la uso kwa sababu ya kukataa kuwakaripia Watu hao.
Hatimaye alikufa mwaka 1440, akatangazwa kuwa Mtakatifu mwaka 1608. Na alipewa jina la Fransiska Romana kwa sabau alikuwa Mroma halisi na hata baada ya kifo chake aliwekwa kuwa msimamizi wa mji wa Roma.

Mtakatifu Fransiska. Utuombee
Watakatifu wote wa Mungu. Mtuombee

 


Current track

Title

Artist

CLOSE
CLOSE