Leo Aprili 13 Kanisa linamkumbuka Mtakatifu Martino wa Kwanza Papa na Mfiadini.

Written by on April 13, 2018

Leo Aprili 13 Kanisa linamkumbuka Mtakatifu Martino wa Kwanza Papa na Mfiadini.
Martino alizaliwa Todi (Italia). Alichaguliwa kuwa Papa mwaka 649. Zamani zile Wamonoteliti wafitini wa dini,walijaribu kutangaza kokote mafundisho yao kwamba Yesu Kristu hakuwa na utashi wa kibinadamu. Katika mtaguso wa Laterani ilithibitishwa kwamba Kristu alikuwa na tashi mbili;utashi wa kibinadamu na utashi wa kimungu.Viongozi wa mafundisho ya uzushi walitengwa na kanisa.
Kaisari Kostansi pamoja na mapatriarki wa Konstantinopoli (Uturuki) na Aleksandria (Misri) waliwasaidia wazushi. Lakini Papa Martino aliitisha mtaguso wa Maaskofu, na wakayapatiliza mafundisho yao. Aliposikia hayo,Kaisari alikasirika sana. Aliwatuma Askari wakamchome Papa kwa kisu wakati wa Misa katika kipindi cha Komunyo. Lakini mwuaji huyo mara alipofuka macho yake hakuweza kumdhuru Papa. Askari mwingine alimkamata Papa alipotoka kanisani na kumpeleka Konstantinopoli (Uturuki). Huko walimtupa gerezani kwa muda wa miezi mitatu. Mashahidi wa uwongo walimshtaki bure, kwamba aliwafitini watu kuwa yeye ,ati, alitaka kumwua Kaisari. Papa huyu hakutaka kusema lolote juu ya mashtaka hayo. Kisha walimsimamisha juu ya kilima, mbele ya watu wakamvua nguo zake za kipapa,halafu wakamtembeza mjini. Mwisho wakamtupa gerezani tena. Punde aliamishwa na kupelekwa kando ya ziwa huko Krimea (Urusi). Alikufa huko kwa ukiwa na njaa mwaka 655.
Mtakatifu Martino wa kwanza ni Askofu wa mwisho wa Roma ambaye anaheshimiwa kama mfiadini mpaka sasa. Aliuawa kwa sababu alipinga mafundisho ya uzushi ya Wamonoteliti.

Mtakatifu Martino. Utuombee
Watakatifu wote wa Mungu. Mtuombee


Current track

Title

Artist

CLOSE
CLOSE