Kardinali Dionigi Tettamanzi, alikuwa ni mtetezi wa Injili ya familia

Written by on August 8, 2017

Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Kardinali Dionigi Tettamanzi, aliyefariki dunia, Jumamosi tarehe 5 Agosti 2017 akiwa na umri wa miaka 83 na mazishi yake yanafanyika, Jumanne, tarehe 8 Agosti 2017, Jimbo kuu la Milano, Kaskazini mwa Italia. Katika salam za rambi rambi alizomwandikia Askofu mkuu mteule Mario Delpini, wa Jimbo kuu la Milano anasema, anapenda kutoa salam zake za rambi rambi kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Jimbo kuu la Milano pamoja na wale wote walioguswa na msiba wa Kardinali Tettamanzi, moja ya viongozi waliopendwa sana na kuthaminiwa na watu kutokana na sadaka pamoja na majitoleo yake katika huduma.

 

Baba Mtakatifu anamkumbuka Marehemu Kardinali Tettamanzi kutokana na mchango wake katika shughuli za elimu na mikakati ya kichungaji alizozitenda. Amekuwa shuhuda mwaminifu wa furaha ya Injili ya Kristo; akalihudumia Kanisa kwa ari na moyo mkuu bila kujibakiza hata kidogo. Tangu alipokuwa Padre wa Jimbo kuu la Milano, alipoteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Ancona-Osimo; kama Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Kwa neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu akaendelea kujisadaka kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Genova na hatimaye, kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano. Baadaye akawa ni Msimamizi wa kitume wa Jimbo la Vigevano.

 

Marehemu Kardinali Tettamanzi katika maisha na utume wake, alijipambanua kuwa ni mchungaji mahiri, aliyejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya mahitaji ya Kanisa la Kristo, kwa mafao ya Wakleri wake na waamini katika ujumla wao. Ni kiongozi aliyesimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya familia inayofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Alijitahidi kufafanua kwa kina na mapana kanuni maadili maumbile, akawa ni “gwiji wa kutupwa” katika medani hii.

 

Mwishoni, Baba Mtakatifu katika salam zake za rambi rambi anasema, anapenda kumwinulia Mwenyezi Mungu sala, ili kwa maombezi ya Bikira Maria, aweze kumpokea mtumishi wake mwaminifu, aliyempenda na sasa amkirimie furaha, amani na maisha ya uzima wa milele. Anatoa baraka zake za kitume kwa wale wote wanaosikitika na kuomboleza msiba wa Kardinali Dionigio Tettamanzi, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Milano, Italia. Anawakumbuka kwa namna ya pekee, waliomsaidia na kumhudumia wakati wa ugonjwa wake, alipokuwa anajiandaa kukunja kilago cha maisha yake hapa duniani!

 

Wasifu wa Marehemu

Kardinali Dionigi Tettamanzi, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Milano, Italia, amefariki dunia, Jumamosi, tarehe 5 Agosti 2017 akiwa na umri wa miaka 83. Kwa sasa Baraza la Makardinali limebaki na jumla ya Makardinali 223 kati yao 121 wana haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na wengine 102 waliobaki hawana tena haki ya kupiga wala kupigiwa kura. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Dionigi Tettamanzi alizaliwa tarehe 14 Machi 1934, Jimbo kuu la Milano. Baada ya masomo na majiundo yake  ya Kipadre akapewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo 28 Juni 1957.

 

Baadaye alipelekwa kujiendeleza kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Gregorian na kujipatia Shahada ya uzamivu katika taalimungu. Kwa muda wa miaka 20 alifundisha taalimungu maadili sehemu mbali mbali za Italia. Katika kipindi hiki akajipambanua kuwa mwandishi mahiri sana wa vitabu kuhusu masuala Injili ya uhai, familia, kanuni maadili na utu wema. Ni kiongozi aliyechangia sana katika mchakato wa shughuli za kichungaji ndani na nje ya Italia.Alikuwa ni kiungo muhimu sana kati ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia na Vatican kuhusu masuala ya Injili ya familia.

 

Tarehe 1 Julai 1989 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Ancona-Osimo na kuwekwa wakfu kuwa Askofu mkuu tarehe 23 Septemba 1989. Aliwahi pia kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Tarehe 20 Aprili 1995 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu Genova. Alibahatika pia kuwa Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Ameshiriki katika maadhimisho mbali mbali ya Sinodi za Maaskofu hapa mjini Roma. Alibahatika kuwa kiongozi mkuu wa Jimbo kuu la Milano kuanzia tarehe 11 Julai 2002 hadi tarehe 28 Juni 2011 alipong’atuka kutoka madarakani. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali tarehe 21 Februari 1998.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

 


Current track
Title
Artist

CLOSE
CLOSE