Askofu Kilaini:Mapadre vijana kuweni na utayari wa kwenda mahali popote Duniani.

Written by on November 14, 2018

Na Izack B Mwacha DSM:

Wito umetolewa kwa Mapadre, kuwa na utayari wa kwenda kila kona ya dunia kuihubiri injili kama ilivyokuwa kwa wamisionari wa kwanza, waliojisadaka maisha yao bila ya hofu yeyete pamoja na kwamba walijua fika hatari pamoja na vitisho vya ajabu sehemu walizokuwa wakienda.

Wito huo umetolewa na Askofu msaidizi wa jimbo katoliki la Bukoba Mhasham Medhod Kilaini wakati akizungumza na Gazeti la kiongozi kwenye makaburu ya wamisionari wa kwanza yaliyopo mlango wa Imani mjini Bagamoyo jimbo katoliki la Morogoro.

Askofu kilaini alibainisha kuwa Vijana ni taifa kubwa kwani wana nguvu na uwezo mkubwa wa kukabiliana na mambo mengi katika utume wao hivyo ni vema Mapadre wote vijana pamoja na watu wote ambao wamejikita katika kuitangaza injili ya kristo kutokuogopa wala kuwa na hofu ya Mazingira ya utendaji kazi kwani anayekuwa msimamizi sahihi katika utendaji wako ni Kristo peke yake.

Akielezea Umuhimu wa kuendelea kuyaeshimu na kuyaenzi makaburi ya Wamisionari hao Askofu kilaini alibainisha kuwa, Pamoja na kwamba waliileta Imani ya kuwakomboa wengi kutoka utumwani lakini pia waliwakomboa kiroho na hatimae msalaba ulisimikwa na moto wa Imani ukawaka tangia kipindi hicho, na hatimae Wengi wao wakapoteza maisha na kuacha mbegu kubwa ya Imani.

Askofu kilaini alifafanua kuwa katika mazingira ya kawaida ni ngumu sana kukubali kufa kwa ajili ya jambo Fulani lakini wamisionari waliotuletea Imani ambayo tunaendelea kuidumisha, bila ya kujali kigezo cha umri mdogo waliokuwa nao, walikubali kuyasadaka maisha yao kwa ajili ya kuipanda mbegu iyo kubwa ya Imani na hivyo kazi kubwa imebaki kwa watu wote kuendelea kuimwagilia ili iweze kusitawi vema.

“Na labda niwahakikishie kwamba Maaskofu tuliohudhuria hapa Zaidi ya Hamsini pamoja na mapadre karibia Elfu moja huku tukiwa na majimbo 34, inamaanisha kabisa bado tunaendelea kuipigania mbegu hiyo ya Imani na tunaimwagilia vema” Alisema Askofu Kilaini.

Akizungumzia Mchakato wa kuwatangaza kuwa Wenye heri na baadae Watakatifu wamisionari wa kwanza Askofu kilaini alibainisha kuwa mtu sahihi mwenye kuwezesha hayo yaweze kufanyika ni kila mtu mwenye Imani, kwa kuomba kwa mwenyenzi Mungu ili yote hayo yaweze kufanyika kadiri ya mapenzi yake.

Ikumbukwe kuwa juma lililopita yalifanyika Maadhimisho ya miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania bara Mjini bagamoyo, yaliyoongozwa kwa kauli mbiu isemayo, FURAHA YA INJILI ambapo pia Baba Mtakatifu Fransic Aliwakilishwa na mjumbe wake maalum Cardinal John Njue ambaye ni Askofu mkuu wa jimbo kuu la Nairobi.

 


Current track

Title

Artist

CLOSE
CLOSE