Taarifa ya Uzinduzi wa Mariathon 2017,

Written by on May 5, 2017

TAARIFA YA UZINDUZI WA MARIATHON 2017

APRILI 28, 2017

Humphrey Julius Kira, Raisi wa Radio Maria Tanzania

 

Mpendwa mdau wa Radio Maria, sauti ya Kikristu Nyumbani Mwako

Tumsifu Yesu Kristu!

Awali ya yote, Napenda kuchukua fursa hii, kwanza kumshukuru Mungu kwa Zawadi ya uhai na Baraka zake. Pili Mama yetu Kipenzi Bikira Maria aliye mlinzi na msimamizi wa Radio yetu, kwa maombezi na usimamizi wake. Nawashukuru mababa Maaskofu wote, Mapadre, Watawa wa kike na wa kiume, Viongozi na Wadau wote wa Radio Maria na taifa zima la Mungu kwa misaada yenu ya hali na mali iliyo iwezesha Radio Maria kufanya utume wake hapa Tanzania kwa kipindi chote cha Miaka 21. Sina la ziada la kusema Zaidi ya neno ‘Asanteni sana’.

Mpendwa msikilizaji wangu, Radio Maria ni chombo cha Uinjilishaji, cha kimisionari chenye lengo la kuitangaza Injili ya Bwana wetu Yesu Kristu kwa watu wote, kila mahali na wakati wote. Kazi za Uinjilishaji ni za gharama, hata hivyo tunapaswa kukumbuka ni wajibu wetu kuitangaza Injili tukiwa kama wakristu wabatizwa. Radio Maria tumejiwekea taratibu mbalimbali za kukushirikisha mdau wetu kuiwezesha Radio yako ili ikuwezeshe kutimiza jukumu lako hilo la Msingi. Hivyo basi, Leo ninakuja kwako kukushirikisha kampeni yetu ya Mbio za Kiroho na Mama yetu Bikira Maria zijulikanazo kama MARIATHON, ambazo nchi zote zenye utume wa Radio Maria hushiriki katika mwezi wa tano, Mwezi wa Mama Yetu Bikira Maria. Hapa Tanzania tutashiriki na Mama yetu katika mbio hizi kuanzia leo tarehe 28/4/2017 na kufikia kilele chake Jumatatu ya tarehe 12/6/2017. Ibada ya Uzinduzi itafanyika Jimboni Iringa siku ya Jumapili tarehe 30/4/2017.

Msikilizaji wangu mpendwa, Mwaka huu tutakuwa tukishiriki Mariathon kwa Mara ya TANO, hivyo sio jambo geni sana masikioni mwetu. Hata hivyo, kutokana na uzoefu tulionao na changamoto mbalimbali zinazo ukabili utume wetu,

inatulazimu mwaka huu kushiriki mbio hizi kwa namna ya pekee kabisa, kila mmoja wetu akijitoa kwa hali na mali kuhakikisha kuwa tunayafikia malengo tunayokusudia ikiwa ni pamoja na kukitangaza chombo hiki kwa watu wengi zaidi, kuongeza Idadi ya marafiki wa Mama ambao daima wamekuwa waaminifu na wakarimu, na chachu ya kuuendeleza utume huu.

 

Msikilizaji wangu, Mariathon ya mwaka jana (2016) tulikuja kwako tukikuomba ukarimu wako katika kukamilisha malengo yetu manne ambayo yalikuwa; Shilingi milioni 40 kwa ajili ya kulipia leseni na vibali mbali mbali vya masafa  kwa mamlaka husika za Mawasiliano kwa Tanzania Bara na Visiwani, Shilingi milioni 90 kwa ajili ya kuendeleza na kukamilisha ujenzi wa Groto la Mama Bikira Maria kwenye Eneo la Studio kuu hapa Mikocheni Dar Es Salaam, Shilingi milioni 75 kwa ajili ya kuhakikisha tunaendelea kuwa hewani kwa kipindi chote cha mwezi Mei 2016, na Shilingi milioni 100 kwa ajili ya malipo ya ada ya Umisionari ambapo Radio Maria zote ulimwenguni zinalo jukumu la kutunisha mfuko huu walao mara moja kwa Mwaka, hivyo Jumla katika Mariathon ya mwaka jana  tulikusudia kukusanya shilingi za Kitanzania milioni 305. Kwa neema za Mungu na Ukarimu wako wa kipekee tulifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi za Kitanzania milioni 386, yaani asilimia 27 zaidi ya lengo letu. Kutokana na ukarimu huo, tulifanikiwa kutekeleza malengo yetu yote kwa asilimia 100 na kubakiwa na kiasi kingine kilichowezesha Radio kuendelea kutoa huduma zake za uinjilishaji.

Mpendwa msikilizaji wangu, mwaka huu tunakuja tena kwako tukiwa na Lengo la kukuomba uiwezeshe Radio yako kiasi cha Shilingi za Kitanzania milioni  450 ambazo ni kwa ajili ya nia zifuatazo; Shilingi milioni 50 kwa ajili ya kulipia ada za masafa ya Radio kwa Tanzania bara na Visiwani, Shilingi milioni 160 kwa ajili ya manunuzi na maboresho ya mitambo yetu, Shilingi milioni 150 kwa ajili ya ada ya Umisionari, na Shilingi milioni 90 kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya Radio kwa mwezi Mei 2017.

Msikilizaji wangu mpendwa, naomba nikufafanulie kidogo kipengele kinachohusu ada ya umisionari. Rejea Lengo msingi la Utume wa Radio Maria ambalo ni kuiwezesha Injili ya Bwana wetu Yesu Kristu kuwafikia watu wote, mahali pote na kila wakati kupitia tekinologia ya Radio. Kumbe basi, kila Mwana familia wa Radio Maria anajukumu, kwanza, kuhakikisha utume huu unaendelea

 

vizuri na bila mawaa katika eneo analoishi, na pili ni kuwa mmisionari kwa kuhakikisha kupitia michango yake ya Ukarimu na Upendo, Kristu anatangazwa Ulimwenguni pote. Hivyo sehemu ya Michango yetu haina budi kuelekezwa katika shughuli za Umisionari, hususani katika maeneo yenye kiu ya kufikiwa na habari njema lakini kutokana na uwezo wa kifedha na hata utulivu wa kisiasa na kijamii hawawezi kupata bahati hiyo bila msaada wako na wangu. Mfano mzuri ni hapa kwetu Tanzania ambapo nasi kupitia mfuko huo wa Umisionari, Radio hii iliweza kutufikia, na zaidi sana, hata baada ya Miaka 21 ya uwepo wake, bado tunaendelea kupokea huduma mbalimbali za uendeshaji zinazo gharamiwa na mfuko huu, mfano gharama za Satelite, misaada ya kiufundi na gharama za mitandao. Fedha za mfuko huo zaidi ya kutumika kusaidia uendeshaji wa Radio Maria ulimwenguni, pia hutumika kwa ajili ya kugharamia miradi mbali mbali ya Uinjilishaji, ambapo mwaka huu mtazamo mkubwa upo barani Afrika na Asia, hususani Mashariki ya Kati. Barani Asia, tunatarajia kuendeleza mradi wetu wa kuanzisha Radio Maria kwa lugha ya Kiarabu katika mji Surat, Parokia ya Erbil, mkoa wa Kurdistan huko IRAQ, ambapo limekuwa eneo la vita kwa muda mrefu sasa na tunao ndugu zetu katika Kristu ambao wana kiu ya kusikia habari njema. Matangazo ya idhaa hii yatazifikia nchi nyingine zinazoongea lugha ya kiarabu ikiwa ni pamoja na Misri, Syria na Jodan. Hayo ni baadhi ya malengo ya mwaka huu ya mfuko huo wa umisionari. Kumbe, kwa kila mchango wako katika kampeni hii utakuwa umefanikisha sehemu ya kila mradi uliokusudiwa na Jumuiya ya Radio Maria Ulimwenguni kwa mwaka 2017.

Msikilizaji wangu Mpendwa, wanafamilia wa Radio Maria Ulimwenguni tumejiwekea utaratibu ambapo kila Mwaka, Mwanachama wa Jumuiya hii huchangia asilimia 10 ya makusanyo yake yote ya mwaka uliotangulia kwenye mfuko huu. Mwaka jana tulifanikiwa kukusanya shilingi Bilioni 1.5 ambapo asilimia 10 yake ni milioni 150 ambazo ndicho kiasi tunachokiomba kwako katika mbio hizi za Mama kama ada yetu ya Umisionari kwa mwaka huu wa 2017.

Msikilizaji wangu mpendwa, kiwango cha milioni 450 kimegawanywa kwa mikoa kama ifuatavyo; (makusanyo halisi ya mwaka jana yamewekwa kwenye mabano); Dar Es Salaam 142m (137m), Arusha 40m (42m), Kilimanjaro 40m (41.5m), Mwanza 40m (32m), Iringa 24m (24.7m), Mbeya 24m (35m), Songea 13m.

(14.5m), Singida 23m (23.6m), Mpanda 6m (6.7m), Mtwara 7m (5.4m), Mbinga 5m (4.4m), Zanzibar 5m (4.0m) na Mikoa mingineyo 17m (10.2m).

Viwango hivyo ni sehemu ya Malengo tuliyo waomba marafiki wa kila mkoa wauwezeshe Utume wa Radio Maria kwa mwaka 2017, hivyo haviongezi malengo ya mikoa, ila kwa kuwa fedha hizi zinahitajika kwa wakati mmoja na ni nyingi, tulionelea ni vyema kuzikusanya katika mwezi huu wa tano, mwezi wa Mama yetu Bikira Maria, kupitia kampeni hii maalum.

Mpendwa msikilizaji wangu, ninayo matumaini makubwa, na furaha pia, kwani palipo na Mama yote yanawezekana. Hata hivyo hatuna budi kufanya kazi kwa bidii, uaminifu, kujituma, pasipo malalamiko na kujitoa bila kujibakiza, huku tukiweka sala mbele ya kila jambo tunalokusudia kulifanya; kwa njia hiyo, tutayaona Maongozi ya Mungu katika kufanikisha nia za Mioyo yetu. Ombi langu la kipekee kwako mpendwa wangu naomba ujitoe kwa moyo wako wote, na kama huna fedha, basi endelea kusali kwa ajili ya mafanikio ya Mbio hizi, kwani sala ni silaha kubwa na muhimu mno kwa mafanikio ya kila jambo, Zaidi sana, jitahidi kuwa balozi mzuri wa Utume wa Radio Maria kwa kuitangaza ili iwafikie watu wengi zaidi.

Mwaka huu tutatembea na Kauli Mbiu isemayo; Utume wa Radio Maria, Kazi ya huruma.

Nakushukuru sana kwa kujitoa kwako na kutenga muda wako adimu kunisikiliza.

 

Ewe Bikira Mwenye huruma………Utuombee

 

Tumsifu Yesu Kristu.

 

………………………………………………….…MWISHO…………………………………………………….

 

Humphrey Julius KIRA,

Raisi, Radio Maria Tanzania

 

NENO LA UZINDUZI

Naomba sasa kutangaza rasmi, kwa unyenyekevu mkuu na matumaini, kwamba Mbio zetu za kiroho pamoja na Mama yetu Bikira Maria zijulikanazo kama MARIATHON 2017 Zimezinduliwa rasmi

na

Usikubali siku hii ya kwanza kabisa ikupite bila kushiriki na Mama.

 


Current track
TITLE
ARTIST

CLOSE
CLOSE