KARIBU RADIO MARIA TANZANIA

TAARIFA MAALUM YA UZINDUZI WA MARIATHON 2015

APRILI 30, 2015

Humphrey Julius Kira, Raisi wa Radio Maria Tanzania

 

Mpendwa msikilizaji wa Radio Maria,iliyo sauti ya Kikristu Nyumbani Mwako, ambaye upo pamoja nami kupitia masafa yetu ya FM, Simu yako ya Kiganjani na au kupitia njia ya Mtandao…..Tumsifu Yesu Kristu!

Nina furaha kubwa kuwa tena pamoja nawe leo hii, ni kiwa na lengo la kukushirikisha mambo mbali mbali kuhusiana na utume huu uliotukuka, ambapo kila mmoja wetu anapata fursa ya kumtangaza Kristu kupitia njia ya tekinolojia ya Radio, na hivyo kutimiza wajibu wetu tukiwa wakristu wabatizwa.Kila Mkristo mbatizwa ana deni la kueneza Injili ya Bwana wetu Yesu Kristo, na tena sio jambo la kujivunia bali ni wajibu wetu. Rejea 1Kor.9:16. (Ninapohubiri Injili, siwezi kujisifu kwa sababu ninalazimika kuhubiri. Ole wangu nisipohubiri Injili.)

Mpendwa Msikilizaji wangu, Napenda kuchukua fursa hii ya pekee kukushukuru sana, kwani siku zote nimekua nikiona miujiza ikitendeka ndani ya Radio yako. Kwa mapendo yako kwa Radio Maria yanayoandamana na majitoleo yako, daima tumekuwa tukiuona wema wa Mungu.Naamini hata wewe msikilizaji wangu umekwisha kuona matendo makuu ya Mungu yakitendeka katika maisha yako kupitia sala na mafundisho mbalimbali yanayotolewa na Radio Maria, na zaidi sana furaha na Amani moyoni unazozipata kwa kuichangia Radio Maria, ili iweze kutimiza malengo yake ya kumtangaza Kristo!

Leo nakuja kwako kukushirikisha kampeni yetu ya Mbio za Kiroho za Mama yetu Bikira maria zijulikanazo kama MARIATHON, ambazo nchi zote zenye utume wa Radio Maria hushiriki katika mwezi wa tano, mwezi wa Rozari takatifu, Mwezi wa Mama Yetu Bikira Maria. Hapa Tanzania tutashiriki na Mama yetu katika mbio hizi kuanzia usiku wa leo tarehe 30/4/2015 hadi tarehe 31/5/2015.

Baada ya Uzoefu mkubwa tulioupata kwenye Mariathon ya mwaka jana pamoja na ile kampeni yetu ya Kapu la Mama, binafsi nimeona mabadiliko makubwa katika utendaji wa Radio yetu, na yote yamekuwa yakifanyika kutokana na moyo wako wa Upendo na majitoleo. Binafsi nimekuwa nikiguswa sana na shuhuda mbali mbali ambazo zimekuwa zikitolewa na wasikilizaji wetu ambazo zinaelezea jinsi Radio Maria ilivyo wagusa mioyo yao, na zaidi sana kuwa sababu ya faraja na furaha katika maisha yao. Kutokana na shuhuda hizo, ni dhahiri kabisa mpendwa msikilizaji, kuwa chombo hiki kilicho chini

ya ulinzi na Usimamizi wa Mama yetu Bikira Maria, daima kinafanya kazi ndani ya mioyo ya wale wenye kuisikiliza na kuikaribisha miujiza midogo inayolenga kubadilisha njia za maisha yao. Radio Maria imekuwa sababu ya kutuwezesha kufanya maamuzi ya kishujaa yenye lengo la kubadilisha mienendo yetu pale Mungu anapo gusa moja kwa moja roho zetu kupitia neno lake.Mpendwa wangu, Haya yote yanatokea kwa Msaada wa Mama yetu Bikira Maria na Neema na Baraka za Mwenyezi Mungu,nasi basi, kwa kutambua hilo, hatuna budi kuonyesha ukarimu wetu kwa kutoa shukrani zetu kwa kuonyesha mapendo kwa wenzetu, kwa njia ya kuwashirikisha ushuhuda wa mambo makuu tunayo yapata kupitia Radio Maria, kuwashawishi nao wawe miongoni mwa wale wanaonufaika na Chombo hiki na zaidi sana kukiwezesha ili kiweze kuendeleza kazi yake ya kumtangaza kristu kila wakati, kila siku na kila mahali katika ulimwengu huu, na tena kwa lugha unayoielewazaidi, huku kikiwalenga wenye shida mbalimbali, wagonjwa, wafungwa na wale wote wasio na watu wa kuwafariji.

Mwaka huu tutakuwa tukishiriki Mariathon kwa Mara ya tatu, hivyo sio jambo geni sana masikioni mwetu. Hata hivyo, kutokana na uzoefu tulionao na changamoto mbalimbali zinazo ukabili utume wetu, inatulazimu mwaka huu kushiriki mbio hizi kwa namna ya pekee kabisa, kila mmoja wetu akijitoa kwa hali na mali kuhakikisha kuwa tunayafikia malengo tunayokusudia ikiwa ni pamoja na kukitangaza chombo hiki kwa watu wengi zaidi, kuongeza Idadi ya marafiki wa Mama ambao daima wamekuwa waaminifu na wakarimu, na chachu ya kuuendeleza utume huu.

Kila Mwana familia ya Radio Maria anamajukumu makubwa mawili , moja ikiwa ni kuhakikisha utume huu unaendelea vizuri na bila mawaa katika eneo analoishi, na pili ni kuwa mmisionari kwa kuhakikisha kupitia michango yake ya Ukarimu na Upendo, Kristu anatangazwa Ulimwenguni pote. Kumbe basi sehemu ya Michango yetu haina budi kuelekezwa katika Umisionari, hususani katika zile Nchi zenye kiu ya kufikiwa na Utume wa Radio Maria, lakini kutokana na uwezo wa kifedha haziwezi kufanya hivyo peke yao. Mfano mzuri ni Tanzania ambapo nasi kupitia michango hiyo ya Umisionari, Radio hii iliweza kutufikia, na zaidi sana, hata baada ya Miaka 19 ya uwepo wake, bado tunapokea misaada toka kwa marafiki na wapenzi wa Radio Maria ulimwenguni.

Mpendwa msikilizaji, zaidi ya malengo mawili niliyoyataja awali, yaani kuongeza wasikilizaji pamoja na marafiki wa Radio Maria, Mwaka huu, tumejiwekea malengo ya kukusanya kiasi cha shilingi milioni 150, ambapo milioni 55 zitatumika kutunisha mfuko wa Umisionari unaoratibiwa na Makao makuu ya Familia ya Radio Maria Ulimwenguni, milioni 55 kwa ajili ya kugaramia matumizi ya kawaida ya Radio yetu kwa mwezi wa tano

na zilizosalia milioni 40 zitatumika kulipia leseni na vibali mbali mbali vya uendeshaji kwa mamlaka husika za Tanzania Bara na Visiwani.

Kiwango cha milioni 150 kimegawanywa kwa mikoa kama ifuatavyo; Dar Es Salaam (57m), Arusha (20m), Mwanza (15m), Moshi (15m), Mbeya (10m), Iringa (10m), Singida (5m), Songea (6m), Mpanda (5m), Mbinga (4m), Mtwara (2m) na Zanzibar (1m).

Viwango hivyo ni sehemu ya Malengo tuliyo waomba marafiki wa kila mkoa watuchangie kwa mwaka huu wa 2015, hivyo haviongezi malengo ya mikoa, ila kwa kuwa fedha hizi zinahitajika kwa wakati mmoja na ni nyingi, tulikusudia wakati wa kuandaa bajeti kuzikusanya katika mwezi huu wa tano, mwezi wa Mama yetu Bikira Maria.

Msikilizaji wangu, mwezi Februari 2015, siku ile ya Wapendanao, nilipokea waraka toka kwa raisi wa Radio Maria Duniani, Mzee wetu Emmanuel Ferario. Katika Waraka wake huo, alitushirikisha jambo ambalo halikuwa la kawaida katika utume wa Radio Maria. Kwa kifupi, baadhi ya fedha ambazo wadau wa Radio Maria Italia walikuwa wakitoa kupitia mapato yao zimesitishwa kutokana na hali ngumu ya Uchumi inayo likabili bara la Ulaya na hivyo Radio Maria Ulimwenguni itapoteza hadi kiasi cha Shilingi Bilioni 4.3 mwaka huu. Fedha hizo ndizo ambazo zimekuwa zikizisaidia Radio Maria mbali mbali ulimwenguni ikiwa ni pamoja na Tanzania kufidia pengo la bajeti ambalo limekuwa likitokana na makusanyo hafifu ya ndani. Kutokana na waraka huo, sasa hatutegemei tena msaada toka Ulaya, inatulazimu kutembea kwa Miguu yetu wenyewe. Katika bajeti yetu ya Mwaka huu tulikuwa tumekusudia kuomba msaada wa shilingi milioni 70 toka makao makuu, hata hivyo kutokana na waraka huo, inatulazimu kuzikusanya wenyewe….hivyo jumla ya makusanyo ya ndani sasa yataongezeka toka milioni 815 hadi milioni 885.

Malengo haya ya Mariathon kwa mwaka huu tayari yalikuwa yamejumuishwa katika bajeti ambayo tuliwashirikisha mwezi Januari 2015, hivyo kufidia pengo la milioni 70 hatuna budi kuchangia zaidi ya malengo yetu!

Nakuomba sana rafiki, mdau na mpenzi wa Radio Maria Tanzania popote pale ulipo, ushiriki kadiri ya ulivyojaliwa na Mungu katika kuhakikisha tunafikia na hata kuyapita malengo yetu haya ili kuhakikisha kazi hii ya kumtangaza kristu inasonga mbele.

Nikiwa kama Raisi na Mtumishi wenu, napenda kuwatia moyo, kutokana na maajabu makuu ya Mungu ninayo yaona yakitokea katika chombo hiki kila siku, kamwe Msiogope, uwezo wa kuiendesha Radio tunao, kwani tunao watu wenye nia ya dhati na Mapenzi ya kweli kwa msimamizi wa Radio Yetu, Mama yetu Bikira Maria. Kumbe basi hatupo peke yetu…tunaye Mama nayetuongoza, kutuelekeza, kutusimamia na kutuombea daima kwa mwanae!

Mpendwa wangu,tumeweza kutembea miezi hii minne ya mwaka huu bila hata senti moja toka kwa wafadhili wanje, na kwa mwelekeo huo, tunayo matumaini makubwa kuwa kwa kuwa tunaye Mama, basi yote yatawezekana. Hata hivyo hatuna budi kufanya kazi kwa Bidii, kujituma, na kujitoa, tena zaidi ya kipindi cha kawaida, huku tukiweka sala mbele ya kila jambo tunalokusudia kufanya, kwa njia hiyo, tutayaona Maongozi ya Mungu katika kufanikisha nia za Mioyo yetu. Kila mmoja ajitoe kwa uwezo wake wote, na hata kama huna fedha, basi endelea kusali kwa ajili ya Mbio hizi, kwani sala ni silaha kubwa na muhimu mno kwa mafanikio ya utume wetu, pia jitahidi kuitangaza Radio yako ili iwafikie watu wengi zaidi.Mpendwa msikilizaji wangu, ili kufanikiwa, binadamu hana budi kupanga vyema na kutekeleza kwa umakini na ueledi mkubwa. Haya huwezekana pale ambapo sala na upendo unaoandamana na nia ya dhati inayojengwa katika misingi ya matamanio mema, vinavyotawala maisha ya huyu binadamu. Kwa kulitambua hilo tumeanzisha ngazi 7 za Uchangiaji ambapo kila mmoja wetu, ataweza kuweka nia za matamanio  moyoni mwake kuifikia pale tutakapo fika tarehe 31/5/2015, kwa kuchangia kidogo kidogo. Siku ya Kilele Michango yako yote itajumuishwa na utajulishwa ngazi uliyoweza kufikia katika mbio hizi za Uinjilishaji. Ili kuweza kujumuisha michango yako, tutakuomba utumie namba moja tuu ya simu kila unapotoa mchango, iwe ni kwa njia ya fedha taslim au kupitia namba yetu 100200..kwani mwishoni tutajumuisha michango yako yote kwa kutumia namba yako ya simu.

Kwa ajili ya Uhamasishaji, na kwa kutambua kuwa tutakuwa tukikimbia pamoja na Mama yetu Bikira Maria,  katika kipindi kizima cha mwezi wa tano, tumeamua kutoa jina kwa kila Ngazi na viwango vyake. Kila kundi litakuwa likiungana na  kiungo kimoja wapo cha Mama yetu ili kumuwezesha aweze kukamilisha mbio hizi salama na kwa mafanikio makubwa.

Naomba nikutajie Makundi hayo pamoja na viwango vyake, ili kuanzia muda huu uanze kujiwekea nia yako Binafsi ambayo ungependa kuifikia au kuivuka pale tutakapo fikia siku ya kilele.

 

Kila mara tutakuwa tukikujuza umeshachangia kiasi gani, na ingawaje hatutajua nia yako ni kufikia ngazi ipi, tutakuwa pia tukikujulisha kiasi kilicho salia kabla hujaingia ngazi nyingine ya juu zaidi. Mungu na akubariki ili uweze kutimiza nia ya moyo wako!

Kauli Mbiu yetu mwaka huu ni ; Tumsaidie Mama Maria naye Atusaidie

Nakushukuru sana kwa kujitoa kwako na kutenga muda wako adimu kunisikiliza.

 Naomba sasa kutangaza rasmi, kwa unyenyekevu mkuu na matumaini, kwamba Mbio zetu za kiroho pamoja na Mama yetu Bikira Maria zijulikanazo kama MARIATHON 2015 Zimezinduliwa rasmi, na namba yetu 100200 kwa mitandao yote sasa ipo wazi!

 Maria Mtakatifu Mama wa Mungu………………Utuombee

Tumsifu Yesu Kristu.

 

 Humphrey Julius KIRA,

Raisi, Radio Maria Tanzania

 

MBIO ZA MAMA MARIA"MARIATHON" KATIKA PAROKIA YA WATAKATIFU PETRO NA PAULO MTWARA.....

 

MKURUGENZI WA MATANGAZO RADIO MARIA TANZANIA PADRE JOHN MAENDELEO, AKITOA MAHUBIRI WAKATI WA MISA TAKATIFU YA UZINDUZI WA MARIATHONI JIMBO KUU KATOLIKI LA DAR ES SALAAM, KATIKA PAROKIA YA WATAKATIFU MASHAHIDI WA UGANDA MAGOMENI...

BAADHI YA WAAMINI WA PAROKIA YA WATAKATIFU WA MASHAHIDI WA UGANDA MAGOMENI WALIOHUDHURIA MISA YA UZINDUZI WA MARIATHON KWA JIMBO KUU KATOLIKI LA DAR ES SALAAM

MWANAFAMILIA NA RAFIKI WA RADIO MARIA NDGU TRASIUS MARKO NGUGO AKIHAMASISHA MBIO ZA MARIATHON KWA MWAKA HUU WA 2015 STUDIO ZA RADIO MARIA MAKAO MAKUU

MWANAFAMILIA WA RADIO MARIA ENGINEER TRASIUS MARKO NGUGO KUTOKA PAROKIA YA MBEZI MWISHO (MT.TERESIA WA MTOTO YESU) AKIHAMASISHA UCHANGIAJI WA MBIO ZA MARIATHON KWA MWAKA 2015

BAADHI YA WANAFAMILIA WA RADIO MARIA WAKIWA KATIKA UZINDUZI WA MARIATHON KWA MWAKA 2015

RAIS WA RADIO MARIA TANZANIA NDUGU HUMPHREY JULIUS KIRA AKIZINDUA RASMI MBIO ZA MAMA YETU BIKIRA MARIA [MARIATHON] MWAKA HUU 2015. KARIBU NAWE USHIRIKI MBIO HIZI KATIKA NAMBA 100200........

 

MKURUGENZI WA RADIO MARIA PADRI JOHN MAENDELEO  AKIZUNGUMZA KATIKA UZINDUZI WA MARIATHON KWA MWAKA 2015..........

 

BAADHI YA MATUKIO MBALIMBALI KATIKA TUKIO LA UZINDUZI WA RADIO MARIA MOSHI

BABA ASKOFU ASAAC AMANI ..WAKATI AKIONGOZA TUKIO LA KUPANDA MTI WA KUMBUKUMBU

TABASAMU BAADA YA KAZI....

Watumishi, Marafiki na wadau wote wa RADIO MARIA TANZANIA wameshauriwa kutumia vema vipaji na karama walizojaaliwa na Mwenyezi MUNGU kwa kufanya utume wa RADIO MARIA kwa upendo na ufanisi   zaidiili wawezekugusa na kuponya Mioyo ya watu.

Ushauri huo umetolewa na Padri JOHN MAENDELEO Mkurugenzi wa matangazo RADIO MARIA TANZANIA wakati akiendesha Mafungo kwa Wafanyakazi, na Marafiki wa RADIO MARIAJimbo Kuu Katoliki la DAR ES SALAAM katika ofisi za makao makuu ya RADIO MARIA AFRIKA Mtaa wa URSINO MIKOCHENI A Jijini DAR ES SALAAM.

Akizungumza katika mafungo hayo ikiwa ni moja wapo ya maadalizi ya MARIATHONI Padri MAENDELEO amesema kuwa ili Utume wa RADIO MARIA uweze kuwa na maana zaidi mbele ya MUNGU na jamii ni vema kila mmoja awe chachu na Dhabihu safi na ya kumpendeza MUNGU mfano wa sadaka safi ya ABEL mtumishi wa MUNGU.

Ameeleza kwamba jambo la msingi na la maana zaidi kwa Watumishi na Marafiki wote wa RADIO MARIA ni kujiweka mikononi mwa MUNGU kwa kusali kila wakati na kufanya utume wa MAMA BIKIRA MARIA kwa upendo na Moyo safi.

Aidha amewataka kutumia muda wao kusoma na keelewa maandiko matakatifu pamoja na karama za utume wa RADIO MARIA ilikuwa chachu kwa wasikilzaji na jamii kwa ujumla.

Radio Maria Kiganjani Mwako

Android Devices
 
Apple Devices
 
Windows Phone Devices